Pembeni yako amesimama mwanamke mzee wa KiKorea, uso wake ukiwa umekunjamana kwa sababu ya miaka mingi ya maisha magumu. Kushoto kwako kasimama kijana mfupi wa Kirusi. Mavazi yake yaliyochakaa pamoja na mikono yake yenye magamba yanakufanya ufikiri kwamba pengine alikuwa mkulima au mfanya kazi kiwandani.
Kama wale wengine wote katika kundi kubwa la watu wanaokuzunguka, hao wawili wanatazama kwa utulivu na ukimya kwenye jukwaa lililoko mbele, mbali kidogo. Wewe uko mahali unapoweza kuona kila kitu japo ni mbali – kiasi cha mita mia kadhaa – na ukiwa hapo unaona jukwaa hilo kuwa linaaribia mita 20 kwa urefu. Linametameta na kung’ara kuliko chochote ulichowahi kuona, kana kwamba limetengenezwa kwa dhahabu na kutiwa katika almasi moja kubwa. Kuna kiti kimoja tu juu yake, ambacho kinaonekana kama kiti cha enzi cha mfalme. Makundi ya watu waliotulia kimya wanatazama kwa mshangao. Bila shaka kuna kitu cha ajabu sana kinachokaribia kutokea hapo.
Unapojaribu kuondoa macho yako na kuangalia pembeni, unatazama makundi ya watu wanaokuzunguka. Ni watu wengi mno kuliko ulivyowahi kuona, na wametanda kwa maili nyingi kila upande. Unakuja kutambua kwamba hakuna ardhi inayo-onekana upande wowote; hata upeo wa macho yako umefunikwa na watu waliofunikwa na jua kana kwamba ni jengo la dhahabu juu yao.
Unapowachunguza wale walio karibu, unaona kwamba ni watu wa kila namna – weupe, wekundu, kahawia na weusi. Kuna waliovaa suti, wengine wamevaa mavazi mbalimbali ya kitamaduni, wengine wachache wamejifunga vitambaa tu kiunoni. Ni kitu kimoja tu ambacho wote wanafanana – ni kwamba wote wametulia kimya, na wote wanasimama wakiwa kama wamenaswa na kitu, wakitazama kile kiti cha enzi cha dhahabu kwa makini sana.
Kuonekana Kwake
Mara sauti inasikika, ikitokea kwenye jukwaa – sauti nzito yenye nguvu na enzi – hujawahi kusikia kitu kama hicho. Mshindo wake ni kama mchanganyiko wa kwaya nyingi pamoja na mvumo wa maanguko makuu ya maji.
Upinde wa mvua unaometa-meta unajitanda juu ya jukwaa, kisha Mtu anatokea, ameketi kwenye hicho kiti cha enzi. Umbo Lake halionekani vizuri, kwa maana anang’aa kama jua. Uwepo Wake kila mmoja anauhisi, na wakati wanapofunika macho yao kutokana na utukufu Wake, wazo moja tu linawafikia wote: Ni msafi — msafi kuliko kijito cha maji safi kabisa au hata theluji iliyo nyeupe mno. Ni mtakatifu. Hakuna kinachoweza kufichwa mbele Yake. Mioyo inaanza kudunda-dunda.
Huyo Mtu mwenye kung’aa anainua mikono Yake juu ikiwa pamoja, kisha anaitenganisha, akiipunga pande zote. Ghafula unahisi nguvu isiyoonekana ikikuinua juu, mpaka unajikuta unaelea pamoja na wengine wengi, juu ya vichwa vya wale wachache waliosalia mahali pao. Kwa pamoja, mnavutwa na nguvu isiyoweza kupingwa kuelekea kulia, na ukitazama wale wengine wachache kwa chini unaona wakivutwa kuelekea kushoto. Baada ya makundi hayo mawili kutenganishwa, nguvu hizo zisizoonekana zinakuweka chini. Humwoni yule mwanamke Mkorea wala yule mwanamume wa Kirusi.
Huyo Mtu mkuu anaanza kuzungumza na kundi la watu walioko kushoto. Sauti Yake haisikiki, lakini ndani yako unasikia tamko Lake. Kutokana na hali ya mshtuko kwenye nyuso za wale wanaokuzunguka, ni dhahiri kwamba kila mmoja anasikia maneno hayo hayo kwa lugha yake mwenyewe. Maneno hayo ni haya:
“Ondokeni kwangu, mliolaaniwa, mwende katika moto wa milele aliowekewa tayari Ibilisi na malaika zake; kwa maana nalikuwa na njaa, msinipe chakula; nalikuwa na kiu, msininyweshe; nalikuwa mgeni, msinikaribishe; nalikuwa uchi, msinivike; nalikuwa mgonjwa, na kifungoni, msije kunitazama” (Mathayo 25:41-43).
Kwa mshangao wa kutisha, lile kundi lililokuwa kimya linajibu kwa pamoja, kwa maswali mengi: “Bwana! ni lini tulipokuona wewe una njaa, au una kiu, au u mgeni, au u uchi, au u mgonjwa, au u kifungoni, tusikuhudumie?” (Mathayo 25:44). Yaani ni kama watakuwa wanasema hivi: “Bwana! Hujawahi kuwa katika hali hizo! Wewe ndiwe Bwana! Tunakuona sasa, unang’aa kama jua; kama tungekuona kabla ya leo, tungekutambua! Una maana gani kusema kwamba tumekwisha kukuona tena, ukiwa na njaa, na kiu, bila makao, bila nguo, ukiwa mgonjwa au hata gerezani?”
Anawajibu na kusema hivi: “Wale walioniamini duniani walifanyika mmoja nami. Walikuwa viungo vya mwili Wangu nami nikaja kukaa ndani yao. Niliweka pendo Langu ndani yao. Kwa hiyo, wanajulikana wazi wale waliokuwa wananiamini Mimi kwa kweli. Walioniamini, waliwapenda ndugu Zangu. Wale waliowachukia ndugu Zangu hawakuniamini Mimi wala hawakunipenda. Na waliowapenda ndugu Zangu walionyesha kwa vitendo upendo wao. Walijali juu ya ndugu zao waliokuwa wanateseka, na walifanya walichoweza ili kupunguza makali ya maumivu yao, hata kama iliwagharimu fedha au wakati. Walijikana wenyewe, wakanifuata Mimi kweli kweli. Hawakufanya mambo hayo ili wajipatie wokovu – walifanya hivyo kwa sababu walikuwa wamebadilishwa na neema Yangu.
“Niliwaonya kuhusu hukumu hii, na maonyo Yangu yanapatikana katika Mathayo sura ya 25. Hamkujali onyo Langu, na sasa mmechelewa. Kweli nawaambia, kadiri msivyomtendea mmoja wa hao ndugu Zangu walio wadogo, hamkunitendea Mimi. Ondokeni kwangu, nendeni katika moto wa milele.”
Hukumu Yenyewe
Maneno Yake ni ya mwisho. Hakuna haja ya kubishana. Inaonekena haiwezekani, lakini ni kweli – umehukumiwa. Unapoanza kuvutwa kurudi chini kwa nguvu mpya ya uvutano, picha zinaanza kupita mawazoni mwako. Kwa pamoja zinakuonyesha mawazo uliyokuwa nayo kuhusu Ukristo, kwamba ni kitu gani:
Ibada kanisani. Nyingi sana – mamia kwa mamia. Sherehe za vyakula za kikanisa. ‘Pikniki’ za kikanisa. Mazoezi ya kwaya kanisani. Vikao vya kamati za kanisa. Mahubiri – mengi sana. Hivi, mchungaji alisema nini juu ya ile hukumu katika Mathayo sura ya 25? Hapo unamwona akiwa amesimama madhabahuni akihubiri: “Hukumu hii ya kondoo na mbuzi si hukumu itakayowahusu Wakristo, bali inahesabiwa na wasomi wengi wa Biblia kuwa ni hukumu ya mwisho ya wasioamini.”
Upuuzi gani! Mbona hatukuona kwamba walikuwepo waamini katika hiyo hukumu ya Mathayo sura ya 25? Mbona hatukuona kwamba lile kundi kubwa la watu kwenye hukumu hiyo ni kutoka “mataifa yote”?
Picha nyingine inakuja akilini mwako – unamsikiliza mhubiri wa redio ukiwa kwenye gari lako kwenda kazini. Akasema hivi: “Hii hukumu ya Mathayo sura ya 25 haipaswi kuogopwa na Mkristo yeyote. Sana sana ni hukumu ya mataifa mbalimbali baada ya Kipindi cha Dhiki Kuu. Mataifa yale yaliyoonyesha wema kwa nchi ya Israeli yataruhusiwa kuingia katika Utawala wa Miaka Elfu Moja. Hayo yanawakilishwa na kondoo. Yale mataifa yaliyowafanyia ubaya Israeli katika wakati wa Dhiki Kuu – yaani mbuzi – watatupwa jehanamu.”
Unapoendelea kuteremka, picha nyingine nyingi zinaingia akilini mwako – za mambo yaliyokula muda wako wote, na nguvu zako na fedha zako ukiwa duniani mpaka ukakosa muda, nguvu au fedha za kuwasaidia Wakristo wanaoteseka. Sasa unaona yote hayo kwa mwanga mpya wa tofauti kabisa:
Kuangalia televisheni na kulipia bili za kukodisha mikanda ya video au kukodisha ‘dishi’ la satelait. Vitu vya kujifurahisha unavyopenda kufanya. Kufuga wanyama kwa starehe tu. Kwenda mapumzikoni – likizoni. Sikukuu za Krismasi – zawadi chungu nzima. Michezo – kushiriki au kuhudhuria. Kununua vifaa vya umeme vipya. Ununuzi wa mavazi kwa kufuata mitindo mipya. Matumizi ya muda na fedha kutazama mtandao wa internet au kwenda kwenye email.
Muda mfupi baadaye unasimama mbele za malango ya jehanamu. Wazo la mwisho linaingia katika akili zako ambazo zinazunguka, kabla ya kitisho chako cha milele kuteka kila eneo la mawazo yako: Je, fedha yote niliyotoa kanisani haikuwa na faida yoyote wala haikuhesabiwa? Dhamiri yako, ambayo wakati huo iko huru kabisa kutokana na uongo wa kale, inakwambia waziwazi kama ifuatavyo: Kanisa lako halikuwa na mpango wa utoaji ili kuwasaidia waamini maskini na wenye kuteseka. Kile kiasi kidogo ulichokuwa unatoa kanisani kilisaidia kulipa madeni ya kanisa, ili muwe na jengo la kufanyia ibada zenu. Pia, fedha yako ililipa madeni ya umeme na maji, ili mpate huduma hizo na kuwa na jengo la kujificha baridi na mvua wakati wa masika, na joto kali wakati wa kiangazi. Pia fedha yako ilisaidia kununua vifaa vya kutumiwa katika Shule ya Jumapili ili watoto wako wawe na kitu cha kujifunza, tena kwa starehe. Pia fedha yako ilisaidia kuwapa posho mchungaji na watenda kazi wa kanisa, ambao muda wao mwingi waliutumia kuhakikisha kwamba ninyi washirika mnafurahia mambo kanisani. Kwa hiyo – fedha yako ilikunufaisha wewe tu, wala haikutolewa kwa sababu ya kumpenda Mungu bali kwa sababu ulijipenda mwenyewe. Tena wewe hukutoa ilivyostahili, kwa hiyo uliwanyonya washirika wengine. Na kile kidogo ulichokuwa unatoa hakikuwa mzigo sana kwako. Hapo unasikia kicheko cha mapepo kikitokea kwenye mapango yaliyoko mbele ya lango la jehanamu.
Jiulize: Kwa mwaka mzima uliopita umelisha Wakristo wangapi wasio na chakula? Je, umewapa waamini wangapi maji ya kunywa, wenye kiu? Ni watoto wangapi wa Mungu wasiokuwa na makao ambao umewasaidia kupata makao? Umewavika Wakristo wangapi nguo ambao hawakuwa na nguo? Au umewatembelea wafuasi wangapi wa Kristo wagonjwa au walio gerezani? Kama ungekufa sasa hivi na usimame katika ile hukumu ambayo Bwana Yesu aliisema katika Mathayo sura ya 25, ungekuwa katika kondoo au mbuzi? Hayo ni maswali mazito kwa wale ambao maisha yao yanafanana sana na yale ya mbuzi.
Ukweli Kuhusu Hukumu Ya Kondoo Na Mbuzi
Je, maonyo ya Yesu katika Mathayo 25:31-46 yanatuhusu sisi? Au alizungumzia hukumu ambayo Wakristo hawahusiki nayo?
Twaweza kuanza kujibu swali hilo kwa kusema kwamba hakika watakuwepo watu waliookoka, waamini Wakristo katika hukumu hiyo. Hakuna awezaye kupinga kwamba wale kondoo walioko kuumeni kwa Yesu si watu waliookoka, tena Wakristo. Wana”urithi ufalme uliotayarishwa tangu kuumbwa ulimwengu” kwa ajili yao (Mathayo 25:34). Wanaitwa “wenye haki” watakaopokea “uzima wa milele” (Mathayo 25:46).
Hoja kwamba kutenganishwa kwa kondoo na mbuzi si kitu kinachohusu watu binafsi bali ni mataifa, kwa sababu ya jinsi wanavyowatendea Israeli wakati wa Dhiki Kuu inaonekana kuwa ngumu kuthibisha kwa kutazama kweli hizo zilizotangulia. Je, tuamini kwamba baada ya sura mbili nzima za maonyo kutoka kinywani kwa Yesu Mwenyewe kuhusu wajibu wa mtu binafsi, atabadilisha maneno sasa na kusema na mataifa ya kisiasa au nchi? Je, anatuonya ili tuhakikishe kwamba tunaishi katika mojawapo ya hizo nchi “kondoo” kama tutakuwa hai wakati wa Dhiki Kuu? Je, tuamini kwamba nchi ile tunayoishimo, bila ya kujali matendo yetu binafsi au maoni yetu juu ya Israeli wakati wa Dhiki Kuu ndicho kitakachoamua kama tutaurithi uzima wa milele au kupotea milele?
Kingine kinachopingana na hoja hiyo kwamba ni mataifa halisi yanatenganishwa badala ya watu binafsi ni ukweli kwamba neno mataifa (25:32) halimaanishi mataifa ya kisiasa hapa duniani, ambayo kwa sasa yamezidi mia mbili. Neno linalotumiwa la Kiyunani – ethne – lina maana ya mbari au makabila, makundi yanayotofautiana kwa sababu ya lugha, utamaduni, mahali walipo na kadhalika. Kama ndivyo, makundi hayo kwa sasa yanazidi elfu kumi hapa duniani. Yesu alisema kwamba mataifa yote watakusanyika mbele Zake” (Mathayo 25:32 – Neno jepesi ni kwa ajili ya kutilia mkazo), kuonyesha kwamba hakuna kundi lolote la kikabila litakalokosekana katika hukumu hiyo. Je, ni sawa kufikiri kwamba atatenganisha makundi ya kikabila kuwa mbuzi na kondoo kwa sababu ya jinsi walivyowatendea Israeli wakati wa Dhiki Kuu? Je, kwa mfano: Atawachukua Wakorea wote kutoka katika mataifa yote wanakoishi, na kuwaruhusu waingie katika Utawala wa Miaka Elfu, ikiwa wengi wao walikuwa wema kwa Israeli wakati wa Kipindi cha Dhiki Kuu? Kadiri unavyoitazama hoja hiyo ndivyo inavyozidi kuwa kituko.
Hoja Nyingine Dhaifu
Je, inawezekana kwamba wale waamini wanaotajwa katika kisa cha Mathayo sura ya 25 ni kundi maalum la Kikristo – kama wale watakaookolewa wakati wa Dhiki Kuu? Labda, lakini wazo hilo hata halitajwi na Yesu kwa mbali. SWALI: Je, uko tayari kujenga wokovu wako juu ya kitu ambacho Yesu hakusema?
Hata tukiamua kwamba ni kundi fulani tu la Wakristo wa Dhiki Kuu ndilo litahusika katika hiyo hukumu ya Mathayo sura ya 25, je kuna sababu yoyote nzuri ya kuamini kwamba wao watahukumiwa kwa kiwango cha juu kuliko wengine wote watakao”urithi ufalme uliotayarishwa tangu kuumbwa ulimwengu” (Mathayo 25:34)? Hapana! Hakuna kibali cha kudhani hivyo, hasa tunapoona kwamba yapo maandiko mengine mengi yenye kusema jambo hilo hilo kwa njia nyingine. Kwa mfano: Katika barua ya kwanza ya Yohana kuna maneno yanayofanana na hayo ya Mathayo 25:31-46. Anasema hivi:
Sisi tunajua ya kuwa tumepita toka mautini kuingia uzimani, kwa maana twawapenda ndugu. Yeye asiyependa, akaa katika mauti … Katika hili tumelifahamu pendo, kwa kuwa yeye aliutoa uhai wake kwa ajili yetu; imetupasa na sisi kuutoa uhai wetu kwa ajili ya hao ndugu. Lakini mtu akiwa na riziki ya dunia, kisha akamwona ndugu yake ni mhitaji, akamzuilia huruma zake, je! Upendo wa Mungu wakaaje ndani yake huyo? Watoto wadogo, tusipende kwa neno, wala kwa ulimi, bali kwa tendo na kweli. Katika hili tutafahamu ya kwamba tu wa kweli, nasi tutaituliza mioyo yetu mbele zake (1Yohana 3:14; 16-19).
Hakuna uwazi kuliko anaotaja Yohana – kwamba, Wakristo wa kweli – yaani wale ambao wamepita kutoka mauti ya kiroho na kuingia katika uhai wa kiroho wanawapenda Wakristo wenzao. Na, upendo ambao Yohana anaandika juu yake si kule kujisikia vizuri tu, bali ni upendo wa kweli unaoonyeshwa kwa matendo – sana sana kwa kutoa mahitaji muhimu ya kimwili. Yohana aliandika kwamba wakati tunapoonyesha upendo wetu kwa ndugu zetu kwa njia hizo, sisi ni “wa kweli” (1Yohana 3:19). Kama tuna jinsi ya kumsaidia mwamini mwenzetu ambaye tunajua ana mahitaji muhimu, na tukaacha kumsaidia, pendo la Mungu halikai ndani yetu, na hatutakuwa na uhakika kwamba tumepita kutoka mautini na kuingia uzimani.
Yakobo Na Yohana Mbatizaji Wanakubaliana
Maneno mengine yanayofanana na yale ya Mathayo 25:31-46 yanapatikana katika Waraka wa Yakobo. Hata yeye alionyesha kwamba upendano wa ndugu, unaoonyeshwa kwa kutoa mahitaji muhimu ni ishara ya imani na wokovu wa kweli. Anasema hivi:
Ndugu zangu, yafaa nini mtu akisema ya kwamba anayo imani, lakini hana matendo? Je! Ile imani yaweza kumwokoa? Ikiwa ndugu mwanamume au ndugu mwanamke yu uchi na kupungukiwa na riziki, na mtu wa kwenu akawaambia, Enendeni zenu kwa amani, mkaote moto na kushiba, lakini asiwape mahitaji ya mwili, yafaa nini? Vivyo hivyo na imani, isipokuwa ina matendo, imekufa nafsini mwake (Yakobo 2:14-17).
Kulingana na Yakobo, imani isiyokuwa na matendo haiwezi kutuokoa. Basi, ni matendo aina gani hasa aliyotaja ili kukazia hoja yake? Matendo ya kuwapa ndugu maskini chakula na mavazi.
Marudio mengine tena ya maneno ya Mathayo 25:31-46 yanapatikana katika mahubiri ya Yohana Mbatizaji. Hakuna anayeweza kupinga kwamba Yohana alikuwa anahubiri mahubiri ya toba na ondoleo la dhambi. Luka anasema hiyo ndiyo “Injili” (ona Luka 3:3, 18). Yohana aliwaonya wasikilizaji wake kwamba kama wasipotubu na kuzaa matunda, mwisho wao ni jehanamu tu (ona pia Mathayo 3:7-12; Luka 3:7-17). Basi, mahubiri ya Yohana ni sawa yakihesabiwa kuwa yenye kutilia mkazo juu ya wokovu.
Alipoulizwa maswali na watu waliochomwa mioyo na mahubiri yake kwamba wafanye nini hasa ili kuonyesha toba yao, Yohana alijibu hivi: “Mwenye kanzu mbili na ampe asiye na kanzu; na mwenye vyakula na afanye vivyo hivyo” (Luka 3:11). Bila shaka Yohana alikuwa anawaita watu watubu ubinafsi au uchoyo wao – hali ambayo ilionekana kwa wao kupuuzia mahitaji makubwa sana ya jirani zao waliokuwa uchi na wenye njaa. Hivi unadhani Yohana angewahakikisha kwamba wameokoka kama wangemjibu kwa kusema: “Sisi tunamwamini Masiya huyo unayesema anakuja hivi karibuni, lakini hatutawahurumia maskini miongoni mwetu”?
Ujumbe Wa Yesu Usiobadilika
Marudio ya maneno ya Mathayo 25:31-46 yanapatikana katika mafundisho mengine ya Yesu. Yule kijana tajiri (ambaye habari zake zinapatikana katika Injili tatu) alikuja kwa Yesu akitafuta uzima wa milele (ona Mathayo 19:16). Yesu alimwambia azishike amri, na akataja sita ambazo yule kijana alidai kwamba amezishika tangu utoto wake. Kisha Yesu akamwambia hivi: “Umepungukiwa na neno moja bado; viuze ulivyo navyo vyote, ukawagawanyie maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha, njoo unifuate” (Luka 18:22). Hicho kilimshinda huyo kijana.
Je, kweli Yesu alikuwa anamwambia ili aingie mbinguni alitakiwa kuuza vitu vyake vyote na kutoa fedha yake kwa maskini? Ndiyo, japo watu wengi wanaona shida kukubali kwamba ni hivyo. Maneno ya Yesu yanayofuata, wakati huyo kijana tajiri anaondoka kwa huzuni, ni haya: “Kwa shida gani wenye mali watauingia ufalme wa Mungu! Kwa maana ni vyepesi ngamia kupita katika tundu la sindano kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu” (Luka 18:24-25. Maneno mepesi ni kwa ajili ya kutilia mkazo). Yesu alikuwa anazungumza kuhusu kuingia mbinguni (ona pia Mathayo 19:23).
Bila shaka maneno ya Yesu hayamhusu yule tajiri mmoja tu aliyeishi miaka elfu mbili iliyopita. Yanawahusu matajiri wote wanaotaka uzima wa milele lakini hawataki kutubu choyo na ubinafsi wao kwa habari ya maskini. Yesu alisema hivi: “Kwa shida gani wenye mali watauingia ufalme wa Mungu!” (Luka 18:24). Isingekuwa “vigumu” kwao kama wasingetakiwa kuachana na mali zao. Lakini kwa sababu wanakataa kuwapenda jirani zao kama wanavyojipenda wenyewe kwa kuwagawia mali kidogo, wanakataa kutubu na kujitolea kwa Mungu na kwa hali hiyo hawawezi kuokoka. Je, hayo si marudio ya Mathayo 25:31-46? Yule kijana tajiri atakuwa miongoni mwa mbuzi.
Ijulikane kwamba Yesu hataki mtu yeyote aamini kwamba anaweza kujipatia uzima wa milele kwa kutoa mali zake zote. Uzima wa milele unapatikana kwa kumwamini na kumfuata Yesu. Hicho ndicho yule kijana alikosa. Kilichomzuia kumfuata Yesu ni mali yake. Fedha yake ilikuwa bwana kwake, kama ilivyoonekana kwa matendo yake. Basi, isingewezekana Yesu awe bwana wake. Kama alivyosema Yesu Mwenyewe: “Hakuna mtu awezaye kutumikia mabwana wawili; kwa maana atamchukia huyu na kumpenda huyu; ama atashikamana na huyu na kumdharau huyu. Hamwezi kumtumikia Mungu na mali” (Mathayo 6:24).
Tena, tunaona kwamba Yesu alimpongeza yule akida Mrumi kwa ajili ya imani yake, akisema kwamba ufalme wa Mungu ungejawa na watu wa Mataifa kama yeye (ona Mathayo 8:10-11). Lakini Yesu hakusema chochote kwake juu ya kuuza vitu vyake vyote na kutoa fedha zake kwa maskini, japo alikuwa tajiri bila shaka. Kwa nini? Ni kwa sababu, kwa upande wake, fedha hazikuwa mungu kwake. Tayari aligawana mapato yake na Wayahudi huko Kapernaumu (kitu cha ajabu kabisa kwa Mrumi kufanya!) kwa kuwajengea sinagogi (ona Luka 7:5). Tofauti na yule kijana tajiri, huyu hakuhitaji kutubia dhambi ya choyo. Inawezekana kabisa kwamba kabla ya kukutana na Yesu alikuwa ameokoka, kama inavyoonekana kwa heshima ambayo wazee wa Kiyahudi huko Kapernaumu walimpa. Kwa kawaida, Wayahudi wangemchukia yeyote anayewakilisha dola ya kigeni iliyokuwa inawatawala.
Sauti Zaidi
Nini ujumbe dhahiri katika kile kisa cha Yesu kuhusu tajiri na Lazaro? Ni huu: Mtu tajiri asiyekuwa na huruma, mwenye kupuuza hali duni ya mtu maskini anayeketi mlangoni pake, anakufa na kwenda jehanamu (ona Luka 16:19-31). Mbuzi mwingine huyo!
Vipi kuhusu mfano wa Yesu juu ya tajiri, katika Luka 12:16-21? Aliuanza kwa maneno haya ya maonyo: “Angalieni, jilindeni na choyo, maana uzima wa mtu haumo katika wingi wa vitu vyake alivyo navyo” (Luka 12:15). Kisha akasimulia kisa chenyewe, hivi:
“Shamba la mtu mmoja tajiri lilikuwa limezaa sana; akaanza kuwaza moyoni mwake, akisema, ‘Nifanyeje? Maana sina pa kuyaweka akiba mavuno yangu’. Akasema, ‘Nitafanya hivi; nitazivunja ghala zangu, nijenge nyingine kubwa zaidi, na humo nitaweka nafaka yangu yote na vitu vyangu. Kisha nitajiambia, Ee nafsi yangu, una vitu vyema vingi ulivyojiwekea akiba kwa miaka mingi; pumzika basi, ule, unywe, ufurahi’. Lakini Mungu akamwambia, ‘Mpumbavu wewe, usiku huu wa leo wanataka roho yako! Na vitu ulivyojiwekea tayari vitakuwa vya nani?’ Ndivyo alivyo mtu ajiwekeaye nafsi yake akiba, asijitajirishe kwa Mungu.”
Ingawa Yesu hakusema mtu huyo alikwenda jehanamu, si halali kufikiri kwamba huyo mchoyo alikwenda mbinguni. Mungu alimwita mpumbavu, kwa sababu wakati wa kifo chake alikuwa tajiri wa mali lakini maskini kiroho. Yesu hakuwa analaumu mafanikio ya mtu huyo, maana ukweli ni kwamba Mungu alihusika kwa sehemu kumletea mafaniko – alituma hali nzuri ya hewa iliyosababisha mavuno mengi tu. Lakini, Yesu alihukumu kile ambacho mtu huyo alifanya na mafanikio yake. Badala ya kufikiri kile ambacho Mungu angetaka afanye na vitu vyake vingi, yeye alijifikia mwenyewe tu, akastaafu mapema na kupanga kuishi maisha ya starehe kwa miaka yake iliyobaki. Usiku huo huo alipofanya uamuzi wake, alikufa. Je, atakuwa kondoo au mbuzi kwenye ile hukumu ya Mathayo sura ya 25?
Yesu alitangaza kwamba wokovu ulifika nyumbani kwa Zakayo baada ya Zakayo kutangaza kwamba angetoa nusu ya mali yake ili kuwapa maskini, na kwamba angemrudishia kila mmoja aliyemdhulumu mara nne (ona Luka 19:8-9). Je, Yesu angeitikiaje kama Zakayo angesema hivi: “Bwana, ninakupokea kama Bwana na Mwokozi wangu, lakini nitaendelea kuwadhulumu watu na kupuuza hali ya maskini”?
Tena, Yesu Mwenyewe aliishi kama alivyohubiri. Kwa vile alikuwa mtii kabisa kwa Torati, bila shaka aliwapa maskini msaada maisha Yake yote. Maandiko yanatuambia aliwapa maskini msaada wakati wa huduma Yake (ona Yohana 12:6; 13:29). Kristo anapokuja kuishi ndani ya mwamini, je, ni yule yule Kristo anayetoa kwa maskini? Bila shaka ndiye. Yesu Mwenyewe alisema hivi: “Amin amin nawaambieni, Yeye aniaminiye mimi, kazi nizifanyazo mimi yeye naye atazifanya …” (Yohana 14:12).
Wakristo Wa Kwanza Walijali Maskini
Maneno ya Mathayo 25:31-46 yanasikika katika kitabu cha Matendo ya Mitume, ambapo tunaona kwamba utunzaji wa maskini kilikuwa kitu cha kawaida katika maisha ya watu wa Agano Jipya. Bila shaka wale wanafunzi wa kwanza walitilia maanani sana agizo la Yesu kwa wafuasi Wake aliposema hivi: “Viuzeni mlivyo navyo, mtoe sadaka. Jifanyieni mifuko isiyochakaa, akiba isiyopungua katika mbingu, mahali pasipokaribia mwivi, wala nondo haharibu” (Luka 12:33). Angalia:-
Na wote walioamini walikuwa mahali pamoja, na kuwa na vitu vyote shirika, wakiuza mali zao na vitu vyao walivyokuwa navyo na kuwagawia watu wote kama kila mtu alivyokuwa na haja. Na jamii ya watu walioamini walikuwa na moyo mmoja na roho moja; wala hapana mmoja aliyesema ya kuwa kitu chochote alicho nacho ni mali yake mwenyewe; bali walikuwa na vitu vyote shirika… na neema nyingi ikawa juu yao wote. Wala hapakuwa na mtu mmoja miongoni mwao mwenye mahitaji; kwa sababu watu wote waliokuwa na viwanja au nyumba waliviuza, wakaileta thamani ya vitu vile vilivyouzwa, wakaiweka miguuni pa mitume; kila mtu akagawiwa kwa kadiri ya alivyohitaji” (Matendo 2:44-45; 4:32-35).
Ona kwamba katika maandiko hayo Luka anataja kwamba neema ya Mungu ilikuwa juu ya hali ya kushirikishana vitu vyote katika kanisa la kwanza. Neema hiyo iliyowasamehe Wakristo wale wa kwanza iliwabadilisha pia.
Maandiko yako wazi kwamba kanisa la kwanza liliwalisha wajane maskini na kuwatimizia mahitaji yao yote ya kimsingi (ona Matendo 6:1; pia 1Timotheo 5:3-10). Je, ni kwa sababu walikuwa wanajaribu kuufanyia kazi wokovu wao? Hapana! Ni kwa sababu walikuwa wametubu dhambi ya choyo na walikuwa wamezaliwa upya na Roho Mtakatifu.
Paulo – mtume mkuu aliyewahi kuishi – aliyepewa na Mungu kazi ya kupeleka Injili kwa watu wa Mataifa, na mwanadamu aliyeandika sehemu kubwa ya nyaraka za Agano Jipya alihesabu sehemu muhimu sana ya huduma yake kuwa ni kuhudumia mahitaji ya kawaida ya maskini. Paulo alichangisha fedha nyingi sana kutoka katika makanisa aliyoanzisha mwenyewe ili kuwasaidia Wakristo maskini. Ona Matendo 11:27-30; 24:17; Warumi 15:25-28; 1Wakor. 16:1-4; 2Wakorintho sura ya 8 na 9; Wagalatia 2:10. Miaka kumi na saba baada ya kuokoka, Paulo alisafiri kwenda Yerusalemu ili kujieleza mbele ya Petro, Yakobo na Yohana kuhusu Injili aliyokuwa amepokea. Hakuna mmoja wao aliyeona hitilafu yoyote na ujumbe aliokuwa akihubiri, na kama Paulo mwenyewe anavyosimulia tukio hilo katika barua yake kwa Wagalatia, anakumbuka hivi: “Ila neno moja tu walitutakia, tuwakumbuke maskini; nami neno lilo hilo nalikuwa na bidii kulifanya” (Wagalatia 2:10). Kwa mawazo ya Petro, Yakobo, Yohana na Paulo, kitendo cha kuwahurumia maskini kinachukua umuhimu wa pili baada ya kuhubiriwa Injili.
Mafundisho Ya Paulo Kuhusu Choyo
Hata Paulo alionya watu kuhusu choyo kwa maneno makali sana. Alifananisha jambo hilo na kuabudu sanamu (ona Waefeso 5:3-5 na Wakolosai 3:5), na alisema wazi kabisa kwamba wachoyo hawataingia katika ufalme wa Mungu.
Lakini uasherati usitajwe kwenu kamwe, wala uchafu wowote wa kutamani, kama iwastahilivyo watakatifu … Maana neno hili mnalijua hakika ya kwamba hakuna mwasherati wala mchafu wala mwenye tamaa, ndiye mwabudu sanamu, aliye na urithi katika ufalme wa Kristo na Mungu. Mtu asiwadanganye kwa maneno yasiyo na maana; kwa kuwa kwa sababu ya hayo hasira ya Mungu huwajia wana wa uasi (Waefeso 5:3, 5-6 – Maneno mepesi ni kutilia mkazo. Ona pia 1Wakor. 5:11; 6:9-11).
Choyo ni nini? Ni shauku ya ubinafsi ya kutaka mali na vitu. Inawezekana kuwa na shauku isiyo ya ubinafsi ya vitu na mali wakati kusudi la mtu ni kutaka kuwapa wengine kile atakachopata. Ukweli ni kwamba mtu hawezi kuwabariki wengine kwa mali kama yeye mwenyewe hajabarikiwa kwanza. Lakini, wakati mtu anapoishi ili apate na kulimbikiza mali kwa starehe yake binafsi – wakati hilo linapokuwa ndiyo lengo lake kuu – ana hatia ya kuwa na choyo (au tamaa ya mali).
Kujipatia Fedha Kwa Uchoyo
Choyo (au tamaa ya mali) ni hali ya moyo, lakini haiwezi kufichika muda mrefu. Kila mara inajitokeza kwa yale watu wanayofanya ili wapate fedha na vitu, na kwa kile wanachofanya na hizo fedha au vitu wakiisha vipata. Hebu kwanza tutazame upande wa choyo unaohusiana na kujipatia. Wakati kupata vitu linapokuwa lengo kuu maishani, mhusika anatenda dhambi hata kama ni tajiri au maskini. Yesu aliwaonya hata waamini maskini kuhusu dhambi hii, wale waliojaribiwa kuwa na wasiwasi kwa sababu ya mambo ya kawaida ya maisha. Alisema hivi:
Hakuna mtu awezaye kutumikia mabwana wawili; kwa maana atamchukia huyu na kumpenda huyu; ama atashikamana na huyu na kumdharau huyu. Hamwezi kumtumikia Mungu na mali. Kwa sababu hiyo nawaambieni, Msisumbukie maisha yenu, mle nini au mnywe nini; wala miili yenu, mvae nini. Maisha je! Si zaidi ya chakula, na mwili zaidi ya mavazi? Waangalieni ndege wa angani ya kwamba hawapandi wala hawavuni wala hawakusanyi ghalani; na Baba yenu wa mbinguni huwalisha hao. Ninyi je! Si bora kupita hao? Ni yupi kwenu ambaye akijisumbua aweza kujiongeza kimo chake hata mkono mmoja? Na mavazi, ya nini kuyasumbukia? Fikirini maua ya mashamba jinsi yameavyo; hayafanyi kazi wala hayasokoti, nami nawaambia ya kwamba hata Sulemani katika fahari yake yote hakuvikwa vizuri kama mojawapo la hayo. Basi, ikiwa Mungu huyavika hivi majani ya kondeni yaliyopo leo na kesho hutupwa kalibuni, je! Hatazidi sana kuwavika ninyi, enyi wa imani haba? Msisumbuke basi mkisema, Tule nini? Au tunywe nini? Au tuvae nini? Kwa maana hayo yote Mataifa huyatafuta; kwa sababu Baba yenu wa mbinguni anajua ya kuwa mnahitaji hayo yote. Bali utafuteni kwanza ufalme wake na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa (Mathayo 6:24-33).
Ona kwamba Bwana Yesu anaanza mafundisho Yake hayo ya Mlimani kwa kuonya juu ya kutowezekana kumtumikia Mungu na fedha. Alisema choyo au tamaa ni sawa na kuzifanya fedha kuwa mungu wetu, yaani, kuruhusu fedha ziongoze maisha yetu badala ya Mungu kufanya hivyo. Yesu aliwaonya wasikilizaji Wake dhidi ya kufanya utafutaji wa hata mahitaji ya msingi kabisa kuwa ndiyo shauku yao kuu. Maneno hayo ni kweli zaidi sana yakihusishwa na hali ya kutafuta vitu visivyo muhimu. Kikubwa cha kutafutwa na wafuasi wa Kristo kinapaswa kuwa “ufalme Wake na haki Yake” (Mathayo 6:33). Wakristo wanaweza kuwa na mambo mengine, na wanatakiwa kutafuta mengine pia. Yesu hakusema “tafuteni tu” bali “tafuteni kwanza”.
Kazi ngumu au bidii ya kazi peke yake si alama kwamba mtu ana tamaa, japo yaweza kuwa. Wakati mtu anapofanya kazi masaa mengi ili aweze kufikia kiwango fulani cha maisha, na upendo wake kwa Kristo uathirike, amekwisha fanya fedha kuwa mungu wake. Mithali ya kale inawashauri watu wanaotumbukia katika hili kwa maneno yafuatayo: “Usijitaabishe ili kupata utajiri; acha kuzitegemea akili zako mwenyewe. Je, utavikazia macho vile ambavyo si kitu? Maana bila shaka mali hujifanyia mabawa, kama tai arukaye mbinguni” (Mithali 23:4-5).
Kujipatia fedha kwa njia isiyo halali au kwa kufuata njia zisizofaa ni vibaya kila wakati, na ni alama nyingine ya tamaa au choyo. Neno la Mungu linasema hivi: “Yeye azidishaye mali yake kwa riba na faida, humkusanyia mtu awahurumiaye maskini” (Mithali 28:8).
Maandiko yanamsifu yule anayeongeza mali yake kwa njia za halali na mwenye kutoa kwa watu kiasi fulani cha mapato yake (ona pia Mithali 13:11; 22:9). Pia, Maandiko yanalaani uvivu na uzembe kwa sababu kadha – moja ikiwa kwamba yule mtu asiye na kipato mwisho wa siku hawi na chochote cha kuwapa wenye mahitaji (ona Waefeso 4:28). Wakati lengo la kupata fedha ni ili kuwa na fedha za kuwagawia wengine, kutafuta fedha kinakuwa kitu chema.
Matumizi Ya Kichoyo Ya Fedha
Sasa hebu tutazame jinsi choyo au tamaa inavyojidhihirisha mara fedha zinapopatikana. Katika hili, choyo au tamaa ni matumizi ya kichoyo ya fedha. Je, ni kitu gani kinachoweza kufanya iwe ni kosa kiadili kwako wewe kutumia fedha yote ambayo umejipatia mwenyewe, kwa ajili yako mwenyewe? Je, ni kwamba wengine – tena wengi katika watoto wa Mungu ambao wanafanya kazi kwa bidii sawa tu na wewe au hata kuliko wewe – au wale wasioweza kufanya kazi – huhangaika ili wapate haidhuru kuishi, wakiwa hawana hata vitu vya msingi kabisa kama chakula cha kutosha hata mlo mmoja? Je, ni sawa kiadili kwamba mtu mmoja anaishi kwa anasa na wengine wanalala usingizi na njaa kila usiku bila kosa lolote?
Zipo sababu nyingi sana za kutofanya chochote ili kuwasaidia waamini ambao ni maskini kabisa – na hata wasioamini – lakini, Wakristo wenye kula vizuri hawatapata rehema wala kuungwa mkono kutoka Biblia. Ingawa hakuna mtu anayeweza kuweka masharti ya mkato kwamba fedha kadhaa itolewe na kadhaa ibaki, Maandiko kwa ujumla yanasema wazi hivi: Wakristo wenye uwezo wa kuwapa watu maskini wanatazamiwa kufanya hivyo na Mungu – hasa kwa waamini wenzao ambao ni maskini kabisa (ona Wagalatia 6:10). Wanaojiita Wakristo wasioonyesha kujali hayo bila shaka ni Wakristo bandia kabisa, na hili ni kundi kubwa sana katika Wakristo wa siku hizi ambao wameingia katika udanganyifu wa kuishi Ukristo wenye kuwatosheleza wao wenyewe kwa sababu ya uchoyo na ubinafsi.
Kulingana na utafiti wa Gallup, ni asilimia 25 tu ya Wakristo wenye kuiamini Injili wanaotoa zaka. Asilimia arobaini wanadai kwamba Mungu ndiye wa maana kuliko chochote maishani mwao, lakini wale wenye mapato ya kuanzia shilingi milioni 50 hadi 75 kwa mwaka hutoa kiasi cha asilimia 1.5 ya mapato yao kusaidia mashirika ya misaada, ikiwa ni pamoja na mashirika ya kusaidia watu ya Kikristo. Wakati huo huo wanatumia asilimia 12 ya mapato yao kwa ajili ya starehe.
Choyo hakionyeshwi tu kwa yale tufanyayo na fedha yetu, bali hata kwa jinsi tunavyotumia muda wetu. Kama wakati wetu wote unatumika kwa mambo ya kibinafsi au starehe, sisi ni wachoyo. Muda ambao Mungu ametupa hapa duniani ni dhamana takatifu sana. Tunapaswa kutumia muda wetu mwingi kiasi iwezekanavyo katika utumishi. Sisi sote – wala si wachungaji tu – tunaweza kutii amri ya Yesu ya kuwatembelea waamini wenzetu ambao ni wagonjwa au wamefungwa gerezani.
Kujitetea Kwa Choyo
Choyo – kama dhambi zingine zote – hujitetea. Hoja moja ni kwamba kwa kuwa tunalipa kodi, na sehemu ya kodi hiyo hutumika kuwasaidia watu maskini, hatuwajibiki kibinafsi kuwasaidia.
Mungu ashukuriwe kwamba serikali zetu zinawajibika kwa kiasi kidogo kuwasaidia maskini. Lakini, sehemu kubwa ya kile kitolewacho na serikali kwa maskini huwa ni kinyume cha mapenzi ya Mungu. Kulingana na Neno la Mungu, maskini wanaoweza kufanya kazi lakini hawataki wanapaswa wasisaidiwe, kama ifuatavyo: “Ikiwa mtu hataki kufanya kazi, basi, asile chakula” (2Wathes. 3:10). Tena, watu maskini ambao ni maskini kwa sababu ya dhambi zao wanatakiwa kwanza waonyeshe toba ya namna fulani kabla ya kusaidiwa. Serikali hazipaswi kutoa fedha ili kuwatia moyo watu wavivu, au wasiowajibika au wenye tabia mbaya. Kwa hiyo, utoaji wetu sisi unatakiwa kuwa tofauti na wa serikali – tukitumia akili vizuri, kwa kusudi la kuendeleza ufalme wa Mungu. Wakati tunapowasaidia maskini wasiokuwa waamini, tunatakiwa pia kuwaeleza habari za Injili. Serikali haifanyi hivyo.
Zaidi – serikali zetu hazifanyi kitu chochote kuwasaidia Wakristo maskini katika nchi zinigne – na hata kama zinafanya, ni kwa sehemu ndogo sana. Sisi tunao wajibu kwa ajili ya familia yetu duniani kote, si kwa wale walioko katika eneo letu tu.
Je, Sisi Ni Maskini Kiasi Gani?
Kujitetea kwingine kunakotokana na choyo yetu ni kwamba wengi wetu wanafikiri sisi ni maskini. Sasa kama ni hivyo, hatutazamiwi kuwasaidia maskini. Lakini, sisi ni maskini kiasi gani? Kulingana na takwimu za Benki ya Dunia, watu bilioni 1.3 duniani wanaishi kwa kipato cha chini ya shilingi elfu moja kwa siku. Wengine bilioni mbili wanaishi kwa kipato kisichozidi shilingi elfu mbili kwa siku. (Mpaka hapo nimezungumza juu ya nusu ya watu wote wanaokaa duniani!)
Kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa, watu bilioni 1.45 hawana huduma za kimsingi za afya. Watu bilioni 1.33 hawana huduma za maji safi ya kunywa, na watu bilioni 2.25 hawana huduma nzuri ya vyoo. Tangu ulipoanza kusoma sura hii, zaidi ya watoto mia tano wamekufa kwa sababu ya njaa au magonjwa yanayoweza kuzuilika. Akina mama mia tano sasa hivi wanaomboleza kwa sababu ya mtoto waliyempoteza dakika ishirini na tano zilizopita kutokana na utapiamlo au ugonjwa unaoweza kuzuiliwa. Kama hatutajali, tuna tofauti gani sisi na yule tajiri aliyempuuza Lazaro?
Mwandishi Mkristo aitwaye Ron Sider katika kitabu chake kiitwacho (tafsiri) Wakristo Tajiri Katika Kipindi Cha Njaa, anakariri maneno ya Robert Heilbroner ambaye “aliorodhesha ‘starehe ambazo ingebidi kuziacha kama tunataka kuishi maisha ya jirani zetu bilioni 1.3 wanaoishi katika umaskini uliokithiri’.” Angalia yafuatayo:
Tunaanza kwa kuvamia nyumba ya familia ya kufikirika tu ya Kimarekani ili kuondoa vitu vyake vya kukalia na kutumia. Kila kitu kiondoke: vitanda, viti, meza, televisheni, taa. Tutawaachia mablanketi machache yaliyochakaa, meza ya chakula, na kiti kimoja cha mbao. Tunabeba makabati pamoja na nguo zake. Kila mwanafamilia anaweza kubakiza “kabatini” mwake suti yake ya zamani au gauni, na shati au blauzi. Tutamruhusu mkuu wa familia kubaki na viatu, lakini mke na watoto hapana.
Twende jikoni sasa. Vifaa vyote vimekwisha tolewa, kwa hiyo tunaingia kwenye makabati … Kiberiti kibaki, mfuko mdogo wa unga, sukari kidogo na chumvi. Viazi vichache ambavyo vimeanza kuharibika na ambavyo vimekwisha tupwa vitafutwe upesi, maana hicho ndicho chakula cha jioni. Tutaacha vitunguu vichache na bakuli la maharage. Vingine vyote tuondoe: nyama, mboga za majani, vyakula vya makoponi, peremende na vitu vingine vitamu kama keki na kadhalika.
Sasa tumesafisha nyumba: birika la bafuni la kuogea limeondolewa, maji ya bomba yamekatwa, waya za umeme zimeondolewa. Sasa tuondoe nyumba. Familia inaweza kuhamia kwenye stoo ya vitu vya kufanya kazi shambani …
Kinachofuata kuondolewa ni mawasiliano. Hakuna magazeti tena, majarida, vitabu – si kwamba vitakosekana maana tumeondoa hata uwezo wa familia kusoma. Badala yake, tunaruhusu redio moja tu …
Halafu, huduma za kiserikali ziondolewe. Hakuna mleta barua, hakuna watu wa kuzima moto. Shule ipo, lakini iko kilomita tatu kutoka nyumbani, na ina madarasa mawili tu … Hakuna hospitali karibu wala daktari. Zahanati ya karibu iko umbali wa kilomita kumi kutoka nyumbani, na anayehusika ni mkunga. Njia rahisi ya kufika huko ni baiskeli, kama familia inayo basi, kitu ambacho si rahisi …
Tumalizie kwa mambo ya fedha. Tunaiachia familia hiyo akiba ya shilingi elfu tano. Hii itamwokoa mkuu wa familia asipatikane na janga lililompata mkulima wa Iran ambaye alipata upofu kwa sababu alishindwa kupata shilingi elfu tatu mia tisa ambazo kwa makosa alidhani anazihitaji ili kupokelewa katika hospitali ambayo angepata matibabu.
Ni Kitu Gani Tusichoweza Kununua?
Hoja yetu kwamba hatuwezi kuwasaidia ndugu zetu na dada katika Kristo ambao ni maskini sana huonekana kuwa unafiki tu kwa kile tunachoweza kutoa fedha kupata: kila mwezi kulipa kodi ya kukodisha huduma ya satelait; malipo ya kila mwezi ili kuletewa magazeti nyumbani, vyakula vya mifugo; starehe za hali ya juu; safari kwenda likizo, magari mapya, kwenda kula nje, mavazi ya mitindo mipya, sigara (kwa wavutaji!), vyakula vya ovyo, vyombo vya kisasa vya umeme pamoja na zawadi nyingi zisizokuwa na maana za Krismasi na sikukuu za kuzaliwa kwa watoto wetu. Hebu tazama nyumbani kwako uone kila kitu ulicho nacho ambacho watu walioishi karne moja iliyopita hawakuwa navyo. Watu walikaa maelfu ya miaka pasipo hivyo vitu tunavyosema sisi “ni vya lazima”, na bado kuna wengi katika sehemu zingine duniani ambao hawana hivyo vitu, na wanaendelea kuishi. Lakini – pamoja na hayo – sehemu kubwa ya mapato ya Wakristo wengi yanakwenda katika vitu hivyo. Na muda wote tukifanya hayo, yule tunayemwita Bwana wetu anapaza sauti Yake akisema, “Msijiwekee hazina duniani, nondo na kutu viharibupo, na wevi huvunja na kuiba; bali jiwekeeni hazina mbinguni, kusikoharibika kitu kwa nondo wala kutu, wala wevi hawavunji wala hawaibi, kwa kuwa hazina yako ilipo, ndipo utakapokuwapo na moyo wako” (Mathayo 6:19-21).
Hali ni mbaya! Si tu kwamba lazima tuwe na vitu ambavyo jirani zetu wanavyo. Imefikia mahali kwamba lazima tuwe navyo sasa, kwa hiyo, tunavinunua kwa mikopo, na hilo linasababisha sehemu kubwa ya fedha yetu iende kwenye kulipia madeni na riba yake. Mara nyingi utakuta kwamba zaidi ya robo moja ya mapato ya watu inaishia kwenye kulipa riba, na mara nyingi ni kwa sababu ya shauku yao ya kutaka kujitosheleza sasa. Je, Mungu atakubaliana na hoja zao kwamba walishindwa kufanya chochote kupunguza makali ya mateso ya watoto Wake maskini?
Sisemi kwamba mtu lazima aishi maisha ya chini ndiyo awe Mkristo. Wala sisemi kwamba ni dhambi kwa Mkristo kuwa na vitu vya kisasa. Maandiko yanafundisha kwamba Mungu “hutupa vitu vyote kwa wingi ili tuvifurahie” (1Timo. 6:1, TLR). Lakini pia Maandiko yanafundisha kwamba Mungu anataka sisi tuwape wengine sehemu ya mali zetu, hasa maskini. Mungu hutubariki – japo kwa sehemu basi – ili na sisi tuweze kuwa baraka kwa wengine.
Kuna wanaotoa hoja kama hii, kwamba: “Lakini, hicho kidogo nitakachoweza kutoa mimi kitafanya nini ukilinganisha na mahitaji ya dunia?” Yaani wanachosema ni hiki: “Mimi siwezi kufanya kila kitu, kwa hiyo sitafanya chochote.” Ukweli ni huu: unaweza kutoa kidogo na kurekebisha au kusaidia sana maisha ya mtu mmoja. Kwa mfano: Ukitoa shilingi elfu mbili kwa siku, unaweza kuongeza mara mbili kipato cha mtu mmoja miongoni mwa wale bilioni 3.3 ambao wanaishi kwa chini ya shilingi elfu mbili kwa siku.
Wengine wanatoa hoja hii: “Mbona Yesu alisema kwamba duniani watakuwepo maskini siku zote? Kwa nini tujitahidi kuondoa kile ambacho Yesu alisema kitakuwepo daima?” Sawa. Kweli Yesu alisema hivi: “Maana sikuzote mnao maskini pamoja nanyi.” Lakini aliendelea na kusema hivi pia: “Na kila mpendapo mwaweza kuwatendea mema” (Marko 14:7). Daima tutakuwa na nafasi ya kuonyesha pendo la Mungu kwa maskini, na bila shaka Yesu alihesabu kwamba – hata kama ni mara moja moja – tutataka kuwatendea mema.
Wengine wanafikiri kwamba wajibu wetu ni kuwasaidia Wakristo maskini tu, na kwamba tunaweza kupuuza hali ya wapagani maskini. Ingawa kweli Maandiko yanatilia mkazo juu ya wajibu wetu kwa waamini wenzetu, hayatuzuii kwamba tuishie hapo tu. Kwa mfano: Mithali 25:21 inasema hivi: “Adui yako akiwa ana njaa, mpe chakula; tena akiwa ana kiu, mpe maji ya kunywa.”
Zipo hoja nyingi nyingine ambazo Wakristo bandia wanatumia ili kutetea ubinafsi wao, lakini hakuna hata moja yenye kubatilisha maagizo ya wazi ya Kristo na Maandiko.
Tufanye Nini?
Itikio pekee linalofaa kwa agizo lolote la Kristo ambalo tunakwenda kinyume nalo ni kutubu. Unaanzia wapi? Anza kwa kufanya tathmini ya kiroho. Kama umeishi maisha ya choyo, basi hujazaliwa mara ya pili. Tubu dhambi zote zinazojulikana maishani mwako na umwite Bwana kwa imani awe Mwokozi wako na Bwana. Mpe Yeye kila kitu na ujitolee kuwa mtumwa Wake.
Kisha, fanya tathmini kifedha. Je, una kipato? Basi unapaswa kuwa ukitoa kiasi fulani. Kiwango cha chini kabisa katika Torati ya Musa kilikuwa zaka, yaani fungu la kumi la kila kitu unachopata. Hapo ni mahali pazuri pa kuanzia kwa kila Mkristo mwenye kipato. Ukiamua kutoa zaka yako yote kwa kanisa lako, hakikisha kwamba kanisa lako lina mpango wa kusaidia maskini mara kwa mara.
Je, huwezi kutoa zaka ya mapato yako? Basi lazima kitu fulani kibadilike. Aidha imekupasa uongeze kipato chako au upunguze matumizi yako. Kwa kawaida, kinachofaa zaidi katika hayo mawili ni kupunguza matumizi. Ndiyo – utahitaji kujikana, lakini hayo ndiyo yanayohusika katika kumfuata Kristo (Mathayo 16:24).
Unawezaje kupunguza matumizi yako? Andika orodha ya kila kitu ulichotumia fedha kwa ajili yake mwezi uliopita. Kisha anza kukata kila kitu ambacho si cha lazima mpaka kiwango cha vitu vilivyokatwa kifikie asilimia kumi ya mapato yako. Usitumie fedha yoyote kwa ajili ya chochote katika hivyo ulivyokata kwenye orodha yako mpaka kipato chako kiongezeke. Halafu, toa hiyo asilimia kumi kama zaka.
Kuondoa Madeni
Kama wewe ni kama watu wengine, bila shaka una madeni mengi tu. Ni hivi: Kama mfuasi wa kweli wa Kristo, unatakiwa kutamani kutoka katika madeni ili uweze kuwa na fedha ya kutoa. Anza kwa kuondoa madeni yenye kutoza riba kubwa, kama yale yatokanayo na kadi za kutoa fedha benki. Zipo njia nne za kupata fedha za kulipia madeni yako, kama ifuatavyo: (1) ongeza mapato yako, (2) uza vitu vyako ambavyo si vya muhimu na lazima, (3) orodhesha tena matumizi yako na uendelee kufuta matumizi yasiyokuwa ya lazima na kuyaondoa kwenye bajeti yako; na (4) punguza matumizi mengine kwa kutumia vitu vizuri. Kwa mfano: Unaweza kupunguza matumizi ya vipasha joto ndani ya nyumba yako wakati wa baridi kwa kuongeza mablanketi zaidi kitandani. Kama watu wangetilia maanani njia hizo nne zote, wangepunguza na kuondoa kabisa madeni yao ya kadi za fedha.
Kama huwezi kutawala matumizi yako ya kadi – na kama una madeni ya kadi inaonyesha huwezi! – basi chukua mkasi uzikate-kate zile kadi.
Baada ya hapo, shughulikia kuondoa madeni yatokanayo na vitu vinavyopungua thamani. Hii unafanya kwa kutumia zile fedha ulizokuwa unalipia riba ya madeni makubwa. Ukiisha maliza kulipa madeni ya vitu vinavyopungua thamani, weka akiba au wekeza zile fedha ulizokuwa unatumia kulipia madeni, na kuanzia hapo, nunua kila kitu kwa fedha taslimu. Yaani – kama huwezi kununua chochote kwa fedha taslimu, usikinunue. Na usinunue kitu usichohitaji.
Kwa kutumia mbinu hizo hizo, shughulika kumaliza madeni yote kwa habari ya vitu vingine vyote.
Mwisho – Weka mpango kuhusiana na mwelekeo wako kifedha kwa miaka iliyobakia ya maishani mwako. Maamuzi yasiyoyumbishwa na ya kutumia akili na yasiyokuwa ya kichoyo yatakusaidia kuwa baraka kwa watu maskini. Zipo njia nyingi za kuishi kwa urahisi tu kwetu sote, zitakazotuwezesha kutoa fedha zaidi. Mfano: Mtu anayenunua magari yaliyokwisha tumika na kulipa fedha taslimu maisha yake yote anaweza kutoa sadaka ya kifedha kubwa tu kwa muda mrefu, kuliko yule anayenunua magari mapya tena kwa kutumia kadi ya mikopo. Ni kweli – japo inategemea uzee wa magari anayonunua na muda anaokaa na kila gari. Tunaweza kufanya maamuzi kama hayo hayo kuhusu nyumba, mavazi, usafiri, vitu vya kufanya, wanyama wa kufuga, zawadi, likizo, tabia zinazoharibu, vyakula na starehe – maamuzi ambayo yatatuwezesha kuweka fedha na hata kutoa maelfu ya shilingi.
Ushauri Kwa Wenye Mali
Vipi kama wewe ni mtu anayejiweza, na una fedha za ziada ambazo umeweka akiba au umewekeza = je, utoe vyote? Kama moyoni mwako unajisikia Mungu amekwambia toa kila kitu, fanya hivyo. Lakini, mapato yanayotokana na uwekezaji wako pamoja na akiba yanaweza kuwa baraka kubwa kuliko wewe kutoa vyote. Mfano: Ikiwa umewekeza kiasi cha shilingi milioni 10 ambazo zinakupa faida ya asilimia 10 kwa mwaka, unaweza kutoa shilingi 1 kila mwaka kwa kipindi chote utakachoishi. Hiyo ni sababu nzuri kwa Mkristo yeyote kufikiria kuwekeza fedha ya ziada anayoweza kuwa nayo mara anapomaliza kulipa madeni yake. Ila, usisahau kwamba, kama mfuasi wa Kristo hupaswi kuwekeza kwenye kitu chochote kisichompendeza Mungu.
Kila mfuasi wa Kristo na hasa wale wenye mali anatakiwa kutambua kwamba Mungu ndiye chanzo cha mali alizo nazo (ona Kumbu. 8:18). Kwa hiyo, mwenye kubariki ana haki kabisa ya kuongoza kile ambacho aliyebarikiwa anapaswa kufanya na baraka zake. Wanafunzi wa kweli wa Kristo wamemkabidhi Kristo mali zao zote. Yesu alisema hivi: “Basi, kadhalika kila mmoja wenu asiyeacha vyote alivyo navyo, hawezi kuwa mwanafunzi wangu” (Luka 14:33). Kila uamuzi wa kifedha ni kitu cha kiroho kwa wale ambao wako chini ya mamlaka ya Yesu kweli kweli.
Wale waliobarikiwa sana wanapaswa kuwa wakarimu mno pia. Paulo alimwandikia hivi Timotheo:
Walio matajiri wa ulimwengu wa sasa uwaagize wasijivune, wala wasiutumainie utajiri usio yakini, bali wamtumaini Mungu atupaye vitu vyote kwa wingi ili tuvitumie kwa furaha. Watende mema, wawe matajiri kwa kutenda mema, wawe tayari kutoa mali zao, washirikane na wengine kwa moyo, huku wakijiwekea akiba iwe msingi mzuri kwa wakati ujao, ili wapate uzima ulio kweli kweli (1Timo. 6:17-19. Maneno mepesi ni kwa ajili ya kutilia mkazo).
Je, ni kiasi gani cha mapato yako unachotakiwa kutoa? Jibu: Kiasi kingi iwezekanavyo! Ninakuhakikishia kwamba utakapofika mbinguni hutajuta kiasi chochote ulichojitoa hapa duniani.
Kadiri unavyojitoa ndivyo utakavyofanana na Kristo. Kumbuka kwamba kiasi cha fedha kinachotolewa si cha muhimu kama kiasi cha kujitoa kinachokuwa katika utoaji wa fedha. Tunasoma hivi katika Injili ya Marko:
Naye [Yesu] akaketi kulielekea sanduku la hazina, akatazama jinsi mkutano watiavyo mapesa katika sanduku. Matajiri wengi wakatia mengi. Akaja mwanamke mmoja, mjane, maskini, akatia senti mbili, kiasi cha nusu pesa. Akawaita wanafunzi wake, akawaambia, Amin nawaambia, Huyu mjane maskini ametia zaidi kuliko wote wanaotia katika sanduku la hazina; maana hao wote walitia baadhi ya mali iliyowazidi; bali huyu katika umaskini wake ametia vyote alivyokuwa navyo, ndiyo riziki yake yote pia (Marko 12:41-44).
Maskini Miongoni Mwetu
Lakini, kutoa kwetu ili kuwasaidia maskini hakuishii kwenye kuandika hundi tu kwa mashirika ya Kikristo. Wapo watu maskini wengi tu wanaoishi karibu nasi. Ni wenye kuhangaika kifedha. Pengine hata wako wanaoshiriki katika kanisa lenu. Unatakiwa kumwuliza mchungaji wako ikiwa kuna yeyote aliye na hitaji kubwa kabisa, ili uweze kutii maneno ya Tito 3:14 – “Watu wetu nao wajifunze kudumu katika matendo mema, kwa matumizi yaliyo lazima, ili wasiwe hawana matunda”.
Mungu ameahidi kuwapa thawabu wale wanaowasaidia maskini, na pia kuwaadhibu wale wanaowapuuza. Ona yafuatayo:
Azibaye masikio yake asisikie kilio cha maskini, yeye naye atalia, lakini hatasikiwa … Mwenye kuwagawia maskini hatahitaji kitu; bali afichaye macho yake atakuwa na laana nyingi (Mithali 21:13; 28:27).
Kisa Cha Kweli
Kwa kumalizia ninataka nikushirikishe mahojiano yanayogusa sana aliyofanyiwa Mkristo maskini anayeitwa Pablito, aliyekuwa anaishi na familia yake pembeni ya dampo kubwa la takataka katika mji wa Manila huko Ufilipino. Mahojiano haya yalichapishwa kwa mara ya kwanza katika gazeti la shirika la Christian Aid litolewalo kila baada ya miezi mitatu liitwalo ‘Utume wa Kikristo’. Mhariri aliweka maelezo yafuatayo ya nyongeza:
Mwaka wa 1985, Umoja wa Makanisa ya Ufilipino ulituma familia ya kimisionari kwenda kwa maskini wa maskini huko Manila ili kufanya huduma. Familia hiyo ni Nemuel na Ruth Palma. Walitumwa kuwafikia watu wanaoishi katika dampo la Manila. Hapo kuna familia mia nyingi zinazoishi katika vibanda tu vilivyojipanga kama viberiti, vilivyoezekwa kwa vipande vya makopo au karatasi chafu za nailoni, na kujengwa na kuta za magunia au vipande vya mbao. Familia ya kawaida tu ya watu saba inakaa katika kibanda ambacho ni bora kidogo tu kuliko nyumba ya kufugia nguruwe, kisichozidi ukubwa wa kitanda cha kawaida tu!
Harufu mbaya iliyopo, na uchafu uliokithiri, na moshi mwingi unaotokana na kuchomwa taka kila wakati, na kuwepo kwa maskani za wezi na watu wakorofi vilimfanya mtumishi mmoja wa Umoja wa Makanisa ya Ufilipino kusema kwamba ni “jehanamu iliyotengenezwa na mwanadamu, mahali ambapo funza hawafi, na moto ni wa kudumu milele.” Ni mahali ambapo panya ni wengi kuliko watoto, na nzi nao ni wengi kuliko panya.
Mahojiano Na Pablito
SWALI: Uliokoka lini?
JIBU: Nilimpokea Yesu kama Mwokozi wangu kwa kushuhudiwa na mtumishi mmoja wa Umoja wa Makanisa ya Ufilipino kama miaka mitano iliyopita. Lakini imani yangu imetiwa nguvu sana kwa shuhuda za watoto wangu watatu wadogo.
Nilipompokea Kristo nilikuwa ‘mmachinga’ wa kuuza sigara zilizoletwa nchini kimagendo. Mara moja nikatambua kwamba hii haikuwa sawa kwa habari ya imani yangu ya Kikristo. Basi nikaacha kufanya biashara hiyo na kuanza kuuza magazeti kwa kuyatandaza njiani.
Lakini tena, ingawa nilikuwa nauza mengi tu na kupata faida kubwa, sikuendelea sana kwenye biashara hii pia kwa sababu niligundua kwamba yalikuwa na picha mbaya na hadithi chafu.
SWALI: Ulianzaje kazi ya kuokoteza kwenye taka?
JIBU: Kweli nilitaka kuishi maisha safi ya Mkristo wa kweli. Basi nikatengeneza mkokoteni mdogo wa mbao nikawa nazunguka mjini Manila kwenye masoko nikiokoteza kwenye majaa ya taka ili nipate angalau chakula kidogo kilichobaki, au chupa zilizotumika, na makopo kwa ajili ya kuuza ili yafanyiwe kazi.
Ukilinganisha na biashara ya sigara na magazeti, hii kazi ni chafu sana tena ya kuchosha. Ninapomaliza siku ninakuwa nimechoka sana na tena ninanuka vibaya sana. Lakini ndani najisikia safi, na hicho ndicho cha muhimu kwangu na kwa familia yangu. Tunataka kuwa na mioyo safi na nia safi mbele za Bwana.
SWALI: Je, maisha yako yaliguswa vipi baada ya watoto wako kumpokea Kristo?
JIBU: Sisi kama familia tuna kajumba kadogo upande wa kusini wa dampo. Ni kibanda tu ambacho kimejengwa kwa kutumia vitu nilivyopata huko, lakini ni nyumba iliyojaa furaha kwa sababu wote tunampenda Bwana. Kila jioni tunafanya ibada kama familia. Binti zangu wanaimba nyimbo ambazo wamejifunza kwenye madarasa ya Biblia. Ninapenda sana kuwasikiliza wakiimba! Wao ni mwanga wa maisha yangu.
Shauku waliyo nayo binti zangu ya kuhudhuria ibada na shule ya Jumapili na kuomba vimetugusa sana mimi na mke wangu. Katika madarasa ya akina Palma wanafundishwa juu ya usafi. Basi, binti zangu wanataka kuvaa nguo safi saa zote.
Pia wanatuhimiza mimi na mama kuvaa nguo safi wakati hatuko kwenye harakati za kuokoteza. Kwa sababu hiyo, familia yetu inaonekana kuwa ya kipekee katika eneo tunalokaa. Jirani zetu wananitania ninapokuwa nimevalia mavazi yangu safi ya Jumapili kwa kuniita “Mwana Sheria”. Mimi hucheka tu kwa sababu ninajua kwamba ndani yao wangependa kuwa safi – ndani na nje pia.
SWALI: Unapataje kukua katika Bwana?
JIBU: Wasichana wetu watatu wanahudhuria mpango wa mafunzo na lishe unaoendeshwa na Nemuel na Ruth Palma. Mke wangu na mimi tunahudhuria kipindi cha kila juma cha mafundisho ya Biblia kinachoendeshwa na akina Palma hapo kwenye dampo letu.
Ninajisikia kumshukuru Bwana kwa kuyafanya maisha yetu kuwa ya furaha licha ya umaskini wetu. Mpaka ninafikia mahali pa kuwaambia wale wenzangu hii furaha. Mimi binafsi ninaendesha somo la Biblia kwa ajili ya jirani zangu, na nimekwisha anzisha somo la Biblia kwa ajili ya watu kumi na mbili wanaokaa upande wa magharibi wa dampo.
Lakini tunahitaji Biblia zaidi. Kitu cha pekee ambacho hatuwezi kupata katika dampo ni Biblia maana hazitupwi. Ila ni ghali pia. (Kila Biblia huko Ufilipino ya kilugha ni kama shilingi elfu nne.)
SWALI: Unawezaje kuishi kwa njia hii ya kuokoteza tu?
JIBU: Kwa kweli kuokoteza hakuna kipato kikubwa. Mtu anaweza kupata kama shilingi elfu moja mia tano kwa siku. Lakini Bwana ametutunza vizuri sana kutokana na dampo la takataka. Unaona hii suruali niliyovaa? Ni nzuri, sivyo? Niliipata kwenye dampo.
Miezi kadhaa iliyopita niligundua kwamba nahitaji miwani ya kusoma. Nikamwomba Bwana, na baada ya siku chache nikaokota hii niliyo nayo! (Hapa, Pablito akaonyesha miwani aliyovaa, ambayo inamshika kwa kutumia kamba). Niliipata kwenye taka zilizokuwa zimetupwa muda si mrefu uliopita. Na miwani yenyewe inalingana kabisa na haja ya macho yangu!
Karibu kila kitu tulicho nacho na tunachotumia – kuanzia mkanda wangu mpaka vifaa vya nywele anavyotumia mke wangu, mpaka viatu na vitu vya kuchezea vya wasichana wangu – vyote tunavipata kwenye dampo hili. Mungu anajua mahitaji yetu madogo, kwa hiyo chochote tunachohitaji hupatikana kwa msaada Wake hapa karibu tu.
SWALI: Ni mabadiliko gani mengine muhimu yaliyotokea maishani mwako?
JIBU: Mimi na Rosita tumejifunza kuyakabili magumu ya maisha kwa tabasamu kwa kuwa Yesu yuko ndani yetu. Tuliacha kutumia lugha chafu, na nilijifunza kuwapenda jirani zangu na kuwasamehe upesi.
Unajua ni kwa nini sina viatu? Jana ilikuwa Jumapili, nami nilipanga kuwahi kanisani ili niwe kwenye kipindi cha maombi. Nikavaa mavazi yangu mazuri na kuvaa viatu vyangu nilivyopata kwenye dampo. Nilitaka kupendeza mbele za Bwana kwa sababu siku mbili tu zilizopita nilisherehekea miaka arobaini na nane tangu kuzaliwa. Kwa hiyo nikajishauri nitumie senti kidogo ili kung’arisha viatu vyangu kwa fundi rangi. Yule fundi rangi akachukua viatu vyangu ili avipige rangi, nami nikawa nimesimama hapo karibu.
Ndipo nikaona maua mazuri kwenye kibanda cha kuuza maua kilichokuwa karibu. Nikaona nimnunulie Bwana maua. Nikavuka mtaa kwenda kununua, niliporudi nikakuta yule mpiga rangi amekimbia na viatu vyangu!
Nilikuwa karibu kulia machozi! Sikushangaa niliposhindwa kukasirika, japo nakiri kwamba nilisikia vibaya wakati nikirudi nyumbani nimevaa nguo zangu nzuri za Jumapili bila viatu, huku nimeshikilia maua mkononi. Jirani zangu walipata nafasi ya kunikejeli sana! Tena, nilichelewa ibada ya asubuhi.
Lakini nilipokuwa naomba kanisani siku hiyo nilitambua kwamba siku moja nitapata jozi nyingine ya viatu ambayo, tofauti na ile iliyoibiwa, itanitosha vizuri kabisa.
Miezi michache baada ya mahojiano hayo, mwandishi habari kutoka shirika la Christian Aid alimtembelea Pablito na kukuta kwamba haokotezi tena. Badala yake, anachota maji kwenye madumu makubwa kutoka kwenye bomba la mtu binafsi kilomita moja kutoka mahali anapokaa, na kuyauza kwa wenzake wanaokaa kwenye dampo kwa fedha kidogo. Akitoa gharama ya kumlipa mwenye bomba, alikuwa anabaki na shilingi elfu moja na mia tano kila siku. Lakini, Pablito alifanya kazi asubuhi tu, tena siku nne kwa juma ili apate nafasi ya kuendesha somo la Biblia mchana na jioni kwa ajili ya watu wanaokaa kwenye dampo kama yeye. Tena Pablito alikiri kwamba mara kwa mara alikuwa anatoa nusu ya mapato yake “kwa maskini”.