Unaruhusiwa kuchapa, kunakili, kugawa au kusambaza haya kwa njia yoyote ile, mradi tu usibadili chochote wala kukata chochote. Vile vile hairuhusiwi kuuza maelezo haya. © Haki zote zimehifadhiwa 2006 David Servant

Sura Ya Ishirini Na Sita
Kufunga

Kufunga ni tendo la hiari la kuacha kula chakula na kinywaji, au kuacha kinywaji, kwa kipindi fulani.

Biblia imeandika mifano mingi ya watu waliofunga. Wengine waliacha kula vyakula vyote na wengine waliacha kula vyakula fulani tu kwa muda wa mfungo wao. Mfano wa hili la mwisho ni ule mfungo wa Danieli wa majuma matatu, ambao hakula “chakula kitamu … nyama wala divai” (Danieli 10:3).

Vile vile kuna mifano michache katika Maandiko ya watu waliofunga kula chakula na maji, lakini aina hii ya mfungo kamili si wa kawaida, na unatakiwa kuhesabiwa kuwa wa kiMungu ikiwa ulizidi siku tatu. Kwa mfano: Wakati Musa alipokaa siku arobaini bila kula wala kunywa chochote, alikuwa mbele za Mungu Mwenyewe mpaka uso wake uling’aa (ona Kutoka 34:28, 29). Alirudia mfungo wa siku arobaini tena, muda mfupi tu baada ya ule wa kwanza (ona Kumbu. 9:9, 18). Hiyo mifungo yake haikuwa ya kawaida, na si vizuri kwa yeyote kujaribu kuiga. Bila ya msaada wa Mungu, haiwezekani kwa mtu kukaa zaidi ya siku chache bila maji. Kuishiwa maji mwilini husababisha kifo.

Hatari kwa afya si kukaa bila maji kwa muda mrefu tu. Hata kuacha kula chakula kwa vipindi virefu huweza kuwa hatari pia, hasa kwa watu ambao wana matatizo ya chakula tayari. Na hata wenye afya nzuri wanapaswa kuwa makini ikiwa wanapanga kufunga kwa muda mrefu zaidi ya wiki moja.

Kwa Nini Watu Wafunge?

Kusudi la msingi la kufunga ni kujipatia muda wa ziada ili kuomba na kumtafuta Bwana. Ukisoma Biblia, hakuna mahali ambapo kufunga kunatajwa bila kuhusisha maombi. Hiyo inatufanya tuseme kwamba kufunga bila kuomba ni kazi bure. Kwa mfano: Katika kitabu cha Matendo, tunasoma sehemu mbili kuhusu kufunga, na kote maombi yanatajwa. Sehemu ya kwanza (ona Matendo 13:1-3), manabii na waalimu katika kanisa la Antiokia walikuwa “wakimfanyia Mungu ibada na kufunga.” Walipofanya hivyo, wakapokea mafunuo ya kinabii, na kwa sababu hiyo wakamtuma Paulo na Barnaba kwenda safari yao ya kwanza ya kimishenari. Katika sehemu ya pili, Paulo na Barnaba walikuwa wanaweka wazee wa kusimamia makanisa mapya huko Galatia. Tunasoma hivi:

Na walipokwisha kuwachagulia wazee katika kila kanisa na kuomba pamoja na kufunga, wakawaweka katika mikono ya Bwana waliyemwamini (Matendo 14:23).

Pengine katika mfano huu wa pili, Paulo na Barnaba walikuwa wanafuata mfano wa Yesu, maana yeye aliomba usiku kucha kabla ya kuchagua wale Thenashara (ona Luka 6:12). Maamuzi muhimu – kama kuchagua viongozi wa kiroho – yanahitaji kuombewa mpaka mtu awe na uhakika kwamba ameongozwa na Bwana. Kufunga kutatoa nafasi nzuri zaidi ya kuomba kwa habari hiyo. Ikiwa Agano Jipya linashauri wanandoa kuacha kushirikiana kimwili ili kuongeza muda wa kuomba (ona 1Wakor. 7:5), basi ni rahisi kuelewa jinsi ambavyo kuacha chakula kwa muda kutafanikisha kusudi hili hilo.[1]

Basi, tunapohitaji kuomba ili Mungu atuelekeze kwa maamuzi muhimu ya kiroho, kufunga ni kitu cha kufanya. Maombi kwa ajili ya mahitaji mengine yanaweza kufanywa kwa muda mfupi sana. (Mfano: Hatuhitaji kufunga ili kuomba sala ya Bwana.) Maombi kwa ajili ya uongozi yanachukua muda mrefu zaidi kwa sababu ya ugumu wetu wa “kusikia sauti ya Mungu.” Kupata uhakika kuhusu maongozi kunaweza kuhitaji maombi ya muda mrefu, na hapo ndipo kufunga kunapokuwa na faida.

Sababu Mbaya Za Kufunga

Kwa kuwa tumetoa sababu za kiMaandiko za kufunga katika Agano Jipya, hebu tutazame sababu zisizokuwa za Maandiko za kufunga.

Kuna watu ambao wanafunga kwa matumaini kwamba itaongeza uwezekano wa Mungu kujibu maombi yao. Sivyo, maana Yesu alituambia kwamba msingi wa kujibiwa maombi ni imani, si kufunga (ona Mathayo 21:22). Tukumbuke kwamba kufunga hakumbadilishi Mungu hata kidogo. Yeye yuko vile vile kabla hatujafunga, na tunapofunga, na baada ya kufunga. Kufunga si njia ya “kumbana Mungu” au namna ya kumwambia, “Lazima ujibu maombi yangu la sivyo nitafunga mpaka nife!” Huko si kufunga KiBiblia – huko ni kugomea chakula! Kumbuka Daudi alifunga na kuomba kwa siku kadhaa ili yule mtoto wake mgonjwa waliyezaa na Batsheba asife, lakini mtoto alikufa kwa sababu Mungu alikuwa anamwadhibu. Kufunga hakukubadilisha hali yake. Daudi hakuwa anaomba kwa imani kwa sababu hakuwa na ahadi yoyote ya kusimamia. Alikuwa anafunga na kuomba kinyume cha mapenzi ya Mungu, kama matokeo yalivyo-onyesha.

Kufunga si sharti la kupata uamsho, kama wengine wanavyofikiri. Katika Agano Jipya, hakuna mfano wa yeyote akifunga kwa ajili ya uamsho. Badala yake tunawaona mitume wakimtii Yesu kwa kuhubiri Injili. Kama mji haukupokea, walimtii Yesu tena, wakikung’uta mavumbi miguuni pao na kusafiri hadi mji uliofuata (ona Luka 9:5; Matendo 13:49-51). Hawakuketi mahali na kufunga, wakisubiri uamsho.

Vile vile kufunga si njia ya “kutiisha mwili” maana shauku ya kula chakula ni kitu halali na wala si dhambi. Angalia katika Wagalatia 5:19-21 uone orodha ya “tamaa za mwili.” Ila, kufunga ni zoezi la kujitawala – au kiasi – na hiyo ni sifa inayohitajika ili kuenenda katika Roho, si katika mwili.

Kufunga kwa kusudi la kuboresha kiroho chako au kutangaza jinsi unavyompenda Mungu ni kupoteza wakati na ni ishara ya unafiki. Hiyo ndiyo sababu iliyowafanya Mafarisayo kufunga, na Yesu aliwasema kwa hilo (ona Mathayo 6:16; 23:5).

Watu wengine hufunga ili kumshinda Shetani. Hilo nalo si Maandiko. Maandiko yanatuahidi kwamba tukimpinga Shetani kwa imani katika Neno la Mungu, atatukimbia (ona Yakobo 4:7; 1Petro 5:8, 9). Hapo kufunga hakupo.

Lakini, si Yesu alisema kwamba kuna mapepo mengine yasiyotoka “isipokuwa kwa kufunga na kuomba”?

Maneno hayo yalisemwa kwa habari ya kumweka mtu huru kutokana na pepo ililokuwa limempagaa, si kwa habari ya mwamini anayehitaji kupata ushindi juu ya mashambulizi ya Shetani kinyume chake.

Swali: Je, maneno ya Yesu hayaonyeshi kwamba tunaweza kupata mamlaka makubwa zaidi juu ya mapepo kwa kufunga?

Kumbuka kwamba wakati baadhi ya wanafunzi wa Yesu walipomwuliza kwa nini wao walishindwa kumtoa mvulana fulani pepo, kwanza alijibu kwamba ni kwa sababu ya imani yao ndogo (ona Mathayo 17:20). Pengine aliongezea, “Namna hii haiwezeani isipokuwa kwa kufunga na kuomba” (Mathayo 17:21), lakini maneno hayo huenda hayakuwepo katika Injili ya Mathayo – yaliongezwa baadaye.

Ila – hata kama Yesu alisema maneno hayo, tutakosea sana kuamua kwamba kufunga kunaweza kuongeza mamlaka ya mtu juu ya mapepo. Kama Yesu atampa mtu mamlaka juu ya mapepo kama alivyofanya kwa wanafunzi Wake kumi na mbili (ona Mathayo 10:1), basi anayo, na kufunga hakuwezi kuyaongeza. Ila, kufunga kunatoa muda zaidi wa kuomba na kutafakari, na kwa njia hiyo kumwongezea imani katika mamlaka yake aliyopewa na Mungu.

Kumbuka kwamba kama Yesu alisema maneno hayo tunayochambua, yalihusu aina moja tu ya pepo. Kufunga bado kungechukua sehemu ndogo sana katika huduma ya ukombozi kwa ujumla, kama basi kuna sehemu yoyote.

Mkazo Kupita Kiasi Kuhusu Kufunga

Kwa bahati mbaya sana, baadhi ya Wakristo wameunda dini kwa habari ya kufunga, wakitoa mahali pakubwa sana katika maisha yao ya Kikristo kwa jambo hilo. Kufungwa hakutajwi hata mara moja katika nyaraka za Agano Jipya.[2] Hakuna mafundisho yatolewayo kwa waamini kuhusu jinsi ya kufunga, au wafunge lini. Watu hawatiwi moyo kufunga. Hii inatuonysha kwamba kufunga ni sehemu ndogo sana katika kumfuata Yesu.

Inaonekana kwamba wakati wa agano la zamani kufunga kulikuwa na mahali pakubwa zaidi. Mara nyingi kufunga kulihusisha na wakati wa maombolezo – kama mtu akifa au wakati wa toba, na wakati wa maombi ya dhati katika vipindi vya matatizo kitaifa au kibinafsi (ona Waamuzi 20:24-28; 1Sam. 1:7, 8; 7:1-6; 31:11-13; 2Sam. 1:12; 12:15-23; 1Waf. 21:20-29; 2Nyakati 20:1-3; Ezra 8:21-23; 10:1-6; Nehemia 1:1-4; 9:1, 2; Esta 4:1-3, 15-17; Zaburi 35:13, 14; 69:10; Isaya 58:1-7; Dan. 6:16-18; 9:1-3; Yoeli 1:13, 14; 2:12-17; Yona 3:4-10; Zekaria 7:4-5).

Vile vile, Agano la Kale linafundisha kwamba kuheshimu sana kufunga na kupuuza kutii amri za muhimu zaidi kama vile kuwajali maskini, ni makosa (ona Isaya 58:1-12; Zekaria 7:1-14).

Bwana Yesu ambaye alifanya huduma Yake wakati wa agano la zamani hawezi kusemwa kwamba yeye alitilia mkazo kufunga kupia kiasi. Alishtakiwa na Mafarisayo kwa kutotilia mkazo wa kutosha (ona Mathayo 9:14, 15). Aliwasema wao kwa kutilia mkazo kupita kiasi (ona Luka 18:9-12).

Lakini pia, Yesu alizungumza na wafuasi Wake kuhusu kufunga, katika mahubiri Yake ya Mlimani. Aliwaagiza wafunge kwa sababu sahihi, akionyeshakwamba aliwatazamia wafuasi Wake kufunga nyakati fulani fulani. Pia aliahidi kwamba Mungu angewapa thawabu kwa sababu ya kufunga kwao. Yeye Mwenyewe alifunga kwa kiasi fulani (ona Mathayo 17:21).

Mtu Afunge Muda Gani?

Mifungo yote ya siku arobaini iliyoandikwa katika Biblia si ya kawaida. Tayari tumetazama habari za Musa na mifungo yake miwili ya siku arobaini, akiwa mbele za Mungu. Eliya vile vile alifunga siku arobaini, lakini kabla ya hapo aliletewa chakula na malaika (ona 1Waf. 19:5-8). Pia, kuna mambo yasiyokuwa ya kawaida kuhusu mfungo wa Yesu wa siku arobaini. Yeye aliongozwa na Roho Mtakatifu kiajabu sana kwenda nyikani. Alipata majaribu yasiyo ya kawaida, kutoka kwa Shetani, alipokaribia mwisho wa mfungo wake. Pia, alitembelewa na malaika alipomalizia mfungo Wake (ona Mathayo 4:1-11).

Ingawa inawezekana kwa watu wengine kufunga kwa siku arobaini pasipo msaada wa Mungu, wengi wanaweza kuwa wanahatarisha afya zao. Mifungo ya siku arobaini si kawaida ya KiBiblia.

Mtu akiacha mlo mmoja kwa hiari yake mwenyewe kwa kusudi la kupata wakati wak umtafuta Bwana, amefunga. Wazo kwamba kipimo cha mifungo ni siku husika ni kosa.

Ile mifungo miwili katika Kitabu cha Matendo tuliyokwisha taja (ona Matendo 13:1-3; 14:23) haikuwa ya muda mrefu. Yawezekana ilikuwa ni mlo mmoja tu.

Kwa kuwa kusudi la kufunga ni kupata muda wa kumtafuta Bwana katika maombi kwa habari ya uongozi Wake, ushauri unaofaa ni kwamba, funga muda wote unaohitaji, mpaka upate mwongozo unaohitaji kwa uwazi. Kumbuka: Kufunga hakumlazimishi Mungu kusema na wewe. Kufunga kunaweza kuboresha usikivu wako kwa Roho Mtakatifu. Mungu anasema na wewe ukifunga na usipofunga. Ugumu tulio nao sisi ni kupambanua maongozi Yake na shauku zetu.

Ushauri Muhimu

Kwa kawaida, kufunga huathiri mwili kwa njia mbalimbali. Mtu anaweza kujisikia udhaifu, uchovu, kichwa kuuma, hali ya kutaka kutapika, kujisikia kulewa, tumbo kuuma na kadhalika. Kama mtu amezoea kunywa kahawa, chai, au vinywaji aina hiyo, baadhi ya mambo yaliyotajwa hapo mbele yanaweza kutokana na kutotumia vitu hivyo katika muda wa mfungo. Kama ni hivyo, ni vizuri kwa watu kama hao kuanza kuacha kutumia vinywaji hivyo siku chache kabla ya mfungo wao. Mtu akizoea kufunga mara kwa mara, atagundua kwamba inakuwa rahisi kufunga kadiri anavyoendelea, japo atajisikia udhaifu fulani.

Mifungo imalizwe polepole, na kama mfungo ulikuwa mrefu, basi mtu awe makini sana kwamba anamalizaje. Kama tumbo la mtu halijasaga chakula kigumu kwa muda wa siku tatu, si vizuri kwake kufungua kwa kula vyakula vigumu. Anapaswa kuanza na vyakula rahisi kusagwa – au vyepesi. Mifungo mirefu inahitaji muda mrefu zaidi kwa tumbo kuanza kuzoea vyakula tena, lakini ukiacha mlo mmoja au miwili huna haja ya kipindi kirefu cha kumaliza mfungo.

Yaliyomo | Sura Iliyopita | Sura Ifuatayo | Mwanzo wa Ukurasa | Pa Kuanzia


[1] Tafsiri nyingi za zamani za 1Wakorintho 7:5 zinaruhusu waume na wake kuacha kuhusiana kimwili ili waweze kujitoa zaidi kwenye “kufunga na kuomba.” Katika tafsiri za kisasa za mstari huu, neno kufunga halipo.

[2] Mahali pekee ni pale Paulo anapotaja kuhusu kufunga kwa wenye ndoa, katika 1Wakor. 7:5, japo hata hapo inategemeana na tafsiri fulani fulani. Kufunga kwa lazima kunatajwa katika Matendo 27:21, 33, 34; 1Wakor. 4:11 na 2Wakor. 6:5; 11:27. Kufunga katika mistari hii hakukuwa kwa sababu za kiroho, bali kwa sababu hali zilikuwa ngumu au kwa sababu hakukuwa na chakula.

 
© Shepherd Serve 2016
The Teaching Ministry of David Servant